Kikosi cha Simba SC kimewasili salama mjini Francistown-Botswana tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy.
Mchezo huo utapigwa kesho majira ya saa kumi jioni kwa saa za Afrika Mashariki katika Uwanja wa Obed Itani Chilume, huku wenyeji Jwaneng Galaxy wakihitaji kuendeleza ushindi kama walivyofanya kwa Wydad Casablanca iliyokubali kufungwa kwao Morocco mwishoni mwa juma lililopita.
Simba SC nayo inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kufufua matumaini ya kuwa sehemu ya timu mbili zitakazotinga Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2023/24, baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani Dar es salaam na Asec Mimosas ya Ivory Coast mwishoni mwa juma lililopita.
Simba SC itacheza kwa mara ya kwanza chini ya utawala wa Kocha Abdelhak Benchikha ambaye analiongoza Benchi la ufundi la klabu hiyo, akichukuwa nafasi ya Robertinho aliyetimuliwa mwanzoni mwa mwezi Novemba.
Wakati Simba SC ikicheza dhidi ya Jwaneng Galaxy, mchezo mwingine wa Kundi B utapigwa huko Ivory Coast kati ya wenyeji Asec Mimosas dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco.