Zimbabwe imekuwa nchi ya pili barani Afrika kufanya mashindano ya urembo kwa wasichana wenye ulemavu wa ngozi (albino), kwa lengo la kupiga vita unyanyapaa na kuelimisha umma kuhusu hali hiyo.
Katika mashindano hayo, mrembo Sithembiso Mutukura aliibuka kuwa mshindi akiwashinda warimbwende wengine 12 waliopanda jukwaani kuwania taji hilo, Ijumaa iliyopita.
Shindano hilo la ‘Beauty Beyond the Skin’ lilifanyika katika klabu ya usiku ya Harare, likifana kama lilivyokuwa shindano la aina hii nchini Kenya.
Mshindi wa shindano hilo, Mutukura amesema kuwa aliamua kushiriki shindano hilo kwa lengo la kutoa elimu, kuongeza uelewa na mtazamo chanya kwa jamii kuhusu watu wenye hali kama yake.
Watu wenye ulemavu huo wa ngozi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya kushambuliwa na kuuawa kutokana na imani potofu za kishirikina katika nchi nyingi barani Afrika.