Mkurugenzi wa klabu ya Udinese ya Italia, Pierpaolo Marino, amedai bodi ya ligi kuu England (EPL), muda si mrefu, itatoa tamko rasmi la kutangaza kuufuta msimu wa 2019-20 kutokana na janga la virusi vya Corona.
Akizungumza na gazeti la Sportitalia, Marino ambaye klabu yake inashirikiana hisa na Watford ya England, ametoa habari hiyo ya mshtuko jana usiku, akidai EPL inatarajia kufuata njia ya Ubelgiji, ambao wiki iliyopita walithibitisha kuufuta msimu wa 2019-20, huku Club Brugge, ikipewa Ubingwa.
“Shirikisho la Ubelgiji tayari limeufuta msimu wa ligi kuu, licha ya kupata vitisho vya UEFA. Huko England, EPL wanakaribia kutoa tamko linalofanana na hilo, kwa sababu hali inazidi kuwa mbaya sana nchini humo. Kiukweli tunatumaini kufurahia tena mpira baada ya virusi vya Corona.
Pierpaolo Marino
“Haijalishi itachukua muda gani kuisha, sisi tunataka kutoka kwenye eneo hatari. Ninahofia msimu ujao, na sio huu wa zamani”. Amesema Marino.
Wakati huo huo viongozi wa ligi kuu Italia, Serie A, wanajadili uwezekano wa kumalizia mechi zote 12 zilizosalia jijini Roma.
Kwa mujibu wa gazeti la La Repubblica, shirikisho la soka nchini Italia, linatafakari kwa kina namna ya kumalizia msimu huu, huku wakipata wazo hilo la kucheza michezo sehemu moja, jambo ambalo halijawahi kufanyika.
Hali mbaya ya virusi vya Corona, imesimamisha shughuli zote za mpira nchini Italia, ingawa bado wana shauku kubwa ya kuona ligi inarejea, hivyo shikirikisho linajiandaa kutengeneza ratiba mpya ya kumalizia msimu huu.