Pierre Liquid, aliyejipatia umaarufu kwa mtindo wake wa kuchekesha baada ya kunywa pombe, ameeleza uzoefu wake na anachoamini kinawafanya watumiaji wengi wa vimiminika hivyo kujikuta wanaamka na ‘hangover’ inayowatesa.
Pierre ambaye ameeleza kuwa yeye hunywa pombe usiku mzima lakini hajawahi kuamka na hang’ over, amesema kuwa wengi wanaokunywa wanashindwa kufuata masharti ya kiafya ya kunywa na kula vizuri.
“Unajua kwa wengi wanaokunywa… kuna jambo moja, mtu anajisahau kula. Anaweza kunywa lakini asile, maji kwake yeye anakuwa ni mvivu kunywa, matunda kwake yeye ni mvivu kula. Kwahiyo wewe ni kula gambe tu lazima ikuathiri. Unaamka asubuhi wewe unapepesuka, ujue tayari imekuathiri,” Pierre alijibu swali la Herith, mwandishi wa habari za afya wa Mwananchi.
Ameeleza kuwa yeye huwa hana haja ya kuamka na kutafuta supu kwani wakati anakunywa ‘vitu’ huhakikisha anakunywa maji kwa wingi na kula mlo mzuri.
Aidha, mtandao wa healthline unaeleza kuwa mtu anapokuwa anakunywa pombe, kila inapofika tumboni, asilimia 20 huingia kwenye damu, na kwamba inapofika kwenye utumbo mwembamba asilimia 75 hadi 85 huingia kwenye mfumo wa damu ambao husambaza athari zake kwenye sehemu mbalimbali za mwili.
Wanaeleza kuwa, mtu anapokuwa amekula vizuri chakula kabla ya kunywa pombe chakula hicho husaidia kuzuia pombe kuingia kwa haraka kwenye utumbo mwembamba. Kama kuna chakula tumboni mwako kabla ya kunywa, pombe huingia kidogo zaidi kwenye mfumo wa damu.