Mshambuliaji wa klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani, Pierre-Emerick Aubameyang inaelezwa kuwa amekubali kuelekea Arsenal katika dirisha dogo la usajili.
Majaaliwa ya Aubameyang yamekuwa hayaeleweki kutokana na matatizo ya kinidhamu kuzidi kuongezeka msimu huu, baada ya kuachwa kwenye kikosi kilichoikabili Wolfsburg kufuatia kukosa mkutano wa timu.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28, amekuwa kwenye rada za timu za England, na mwezi huu alikuwa akitajwa kuingia kwenye rada za klabu za China.
Hata hivyo vyombo vingine vya habari vimeripoti kuwa, Aubameyang amefikia makubaliano na Arsenal kwa mkataba ambao utamfanya kuwa mchezaji anayelipwa dau nono zaidi katika historia ya klabu.
Uhamisho wake utategemea kuondoka kwa Alexis Sanchez mwezi huu, na mchezaji huyo wa kimataifa wa Chile yupo mbioni kujiunga na Manchester United baada ya kufikia makubaliano na miamba hao wa Old Trafford.