Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa Pierre Liquid ataambatana na Timu ya Taifa, Taifa Stars katika fainali za AFCON zitakazofanyika nchini Misri.
Ameyasema hayo wakati akizungumza naye katika Viwanja vya Bunge Jijini Dodoma, ambapo Piere alikwenda kutembelea kwa mwaliko wa Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Hayo yamejiri ikiwa zimepita siku chache tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda kutoa kauli ya kukosoa tabia ya watu kuvipa muitikio mkubwa vitu visivyo na msingi, akitolea mfano wa mchekeshaji huyo aliyejizolea umaarufu kwenye vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii.
Aidha, katika hafla iliyoandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo ambayo ilikuwa na malengo ya kutokomeza ziro katika wilaya hiyo, Makonda alisema kwamba watu wa ‘hovyo’ kama Pierre hawapaswi kupewa nafasi kwenye vyombo vya habari, hali iliyozua gumzo kubwa.
“Wakina mama kama hawa wanaojituma na kuhangaika kwa ajili ya watoto, wao ndio tuwape kipaumbele, sio hawa walevi walevi, yaani unakuwa na taifa ambalo watu wa hovyo ndio wanakuwa maarufu,”alisema Makonda