Mshambuliaji Wayne Rooney ataukosa mchezo wa robo fainali ya kombe la chama cha soka nchini England (FA Cup), ambapo Man Utd watapambana na Chelsea leo usiku kwenye uwanja wa Stamford Bridge.
Rooney hatokuwa sehemu ya kikosi cha Man Utd kufuatia jereha la mguu linalomkabili, baada ya kugongana na beki, Phil Jones wakiwa kwenye mazoezi ya kuelekea mchezo huo ambao utaunguruma ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka duniani kote.
Jopo la madaktari la Man Utd limejiridhisha kwa kina kuhusu jeraha la mshambuliaji huyo, na imebainika hatoweza kucheza mchezo dhidi ya Chelsea.
Kuumia kwa Rooney, kunampa wakati mgumu meneja wa Man Utd, Jose Mourinho ambaye itamlazimu kutumia mbinu mbadala ya kuifumua safu yake ya ushambuliaji katika mchezo wa leo.
Tayari imeshafahamika mshambuliaji wake kutoka nchini Sweden Zlatan Ibrahimovic hatocheza mchezo huo, kufuatia adhabu ya kufungiwa michezo mitatu iliyotolewa na chama cha soka nchini England (FA), kutokana na utovu wa nidhamu aliouonyesha katika mchezo wa ligi dhidi ya AFC Bournemouth.
Washambuliaji wengine kama Anthony Martial na Marcus Rashford nao wanakabiliwa na majeraha.
Duru zinasema huenda meneja huyo kutoka nchini Ureno akamtumia kiungo Marouane Fellaini kama mshambuliaji katika mpambano dhidi ya Chelsea, kutokana na mchezaji huyo wa Ubelgiji kuwahi kucheza nafasi hiyo akiwa na klabu yake ya zamani ya Everton.
Wachezaji wengine wa Man Utd ambao watashindwa kucheza mchezo dhidi ya Chelsea kwa sababu za kuwa majeruhi ni Bastian Schweinsteiger, Henrikh Mkhitaryan na James Wilson.