Pikipiki 20 alizozitoa Diamond Platinumz mwishoni mwa mwaka jana katika maeneo ya Tandale jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwasaidia vijana kujiajiri zimepotelea mikononi mwa ‘wapigaji wachache’.
Bosi huyo wa WCB alitoa pikipiki hizo kwa sharti kuwa watakuwa wakirejesha kidogo-kidogo ili ziweze kuzalisha pikipiki nyingine na kutoa fursa kwa vijana wengi zaidi. Lakini kwa mujibu wa Meneja wake, Babu Tale, mpango huo umekuwa tofauti.
“Kwa kifupi naweza kusema watu wasiokuwa na nia njema na maendeleo wameamua kugawana pikipiki hizo. Tumejaribu kufuatilia tukaona tutajenga uhasama bure wakati lengo lilikuwa kutoa msaada,” Babu Tale ameliambia gazeti la Mwananchi.
Sambamba na pikipiki hizo, Diamond alitoa kadi ya bima ya afya kwa wananchi 1,000 pamoja na msaada wa bajaji kwa mwanamke mmoja mlemavu.
Diamond alimuona mwanamke huyo kupitia Wasafi TV ambayo inaruka mtandaoni. Alisema aliguswa na simulizi la mwanamke huyo na akaamua kumsaidia.
Babu Tale alifunguka kuwa wakati ambapo Diamond anafikiria kupiga hatua na kuwasaidia vijana wenzake, watu wengine walikuwa wanafikiria namna ya kumuangusha.