Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda amewaasa watanzania hususan vijana wanaopatiwa mafunzo ya unenepeshaji mifugo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambapo baada ya mafunzo hayo ya mwaka mmoja kila mmoja ataondoka na mtaji usiopungua Shilingi Milioni Kumi za ufugaji wa kibiashara.
Pinda ameyabainisha hayo wakati alipofanya ziara ya siku moja Mkoani Tanga, kutembelea vituo atamizi vya wizara hiyo vinavyotekelezwa kupitia Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa ajili ya kutoa mafunzo ya vitendo ndani ya mwaka mmoja kwa vijana juu ya unenepeshaji ng’ombe katika kipindi cha miezi mitatu.
“Kilimo hiki au ufugaji huu ni biashara kwa uhakika, ng’ombe uliyemnunua Laki Mbili (2) unakuja kumnenepesha kwa miezi mitatu baadaye unakuja kumuuza Milioni Mbili kwa nini usihangaike nalo hili?, Mwaka mzima unaniachia Milioni Kumi kwa nini nisifanye?” amesema Pinda.
Ameongeza kuwa ufugaji wa kibiashara ni muhimu kwa vijana hao kuzingatiwa kwa kutoa elimu waliyopata kwa wafugaji ya namna bora ya kuchagua mifugo minadani na kuipatia malisho bora vikiwemo vyakula vya ziada ili kuwanenepesha na kuuza kwa faida baada ya miezi mitatu.