Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imetupilia mbali pingamizi lililowekwa na Mawakili wa Utetezi katika Kesi ya Ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake 3.
Jaji Joachim Tiganga amekubaliana na hoja za upande wa Mashtaka na kukubali barua iliyotolewa na Naibu Msajili wa Mahakama itolewe kama kielelezo na shahidi namba mbili katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi.
Mawakili upande wa utetezi walipinga kuhusiana na barua ambayo upande wa mashtaka uliomba kuiwasilisha kupitia shahidi wa pili katika kesi hiyo ndogo.
Upande wa mashtaka Ijumaa iliyopita kupitia kwa shahidi huyo wa pili uliiomba mahakama iipokee barua hiyo ya msajili inayoonesha kuwa upande wa mashtaka umeomba kitabu cha kumbukumbu za Mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam cha mwaka 2020, ili shahidi huyo aweze kukiwasilisha mahakamani hapo kama sehemu ya ushahidi wake na kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.