Mabingwa wa Soka Barani Afrika klabu ya Al Ahly wametangaza kusitisha mkataba wa winga kutoka nchini Angola, Geraldo da Costa – Geraldo aliesajiliwa klabuni hapo Januari 2019 akitokea CD 1º de Agosto kwa usajili uliogharimu kiasi cha dola za kimarekani 800,000.
Usajili wa mshambuliaji kutoka nchini Zambia Walter Bwalya, unatajwa kuwa kichocheo kikubwa cha kuondoka kwa mshambuliaji huyo ambaye alikua sehemu ya kikosi cha Al Ahly kilichocheza dhidi ya Zamalek katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika (CAF Champions League).
Kocha wa Mabingwa hao wa Misri, Pitso Mosimane amethibitisha kutoridhishwa na kiwango cha Geraldo tangu alipowasili klabuni hapo mwishoni mwa mwaka jana, na mara moja aliwasilisha pendekezo la kutaka aachwe kwenye usajili wa kipindi hiki cha kuelekea hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Geraldo alianza vizuri maisha mjini Cairo, akifunga mara tatu wakati akisaidia magoli sita katika michezo 17, pamoja na goli la ushindi muhimu wa dakika za mwisho dhidi ya Smouha, alicheza na Kuwa na jukumu kubwa katika kusaidia Klabu kushinda taji la ligi la 2018/19.
Katika msimu wake wa kwanza kamili na Al Ahly, Geraldo hakuweza kuwa na Kiwango chake kutoka msimu wake wa kwanza na alifunga mara mbili tu katika michezo 25.
Kwa jumla akiwa na Al Ahly, Geraldo alifunga mabao matano na kutoa assist saba katika michezo 45, akiisaidia timu hiyo kushinda mataji mawili ya ligi, Kombe la Misri, na Ligi ya Mabingwa Afrika – Kabla ya muda wake huko Misri, Geraldo alikuwa amecheza kwenye vilabu vya Brazil, Coritiba, Paraná Clube, Red Bull Brasil, Atlético Clube Goianiense, na CD 1º de Agosto ya kwao Angola.
Kwenye kiwango cha kimataifa, Geraldo ana Michezo 27 kwa timu yake ya taifa ya Angola, akifunga mara mbili na akishiriki katika michezo yao yote mitatu kwenye AFCON ya Mwaka 2019.