Makamu mwenyekiti wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia alikuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Pius Msekwa ametoa tathmini yake kuhusu hali ya kisiasa nchini hususan kutokana na ushindani mkali ulioshuhudiwa katika mbio za urais mwaka Jana.

Msekwa ameeleza kuwa kutokana na kuungana kwa vyama vya upinzani vilivyounda Ukawa, umoja huo uliimarika na ndio sababu ya kutoa ushindani mkali kwenye uchaguzi huo tofauti na chaguzi nyingine, huku akieleza kuwa chama chake kimekuwa na historia ya kupanda na kuporomoka.

Alielezea historia ya ushindi wa urais wa makada wa CCM kwa mihula tofauti tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi japo imeendelea kuwa madarakani.

“CCM inapanda na kuporomoka,” Msekwa aliliambia gazeti la Rai. “Kwa mara ya kwanza Mkapa alishinda kwa asilimia 61,lakini hali ilikuja kubadilika katika awamu ya pili, alishinda kwa asilimia 71,” aliongeza.

Alisema Rais Kikwete aliingia kwa ushindi wa kishindo wa asilimia 82 lakini uchaguzi uliofuata alishuka na kupata asilimia 61 kulingana na hali ilivyokuwa kisiasa.

Akimzungumzia ushindi wa Rais John Magufuli wa asilimia 58 ambao ni mdogo zaidi katika historia ya chama hicho, alisema ulitokana na nguvu na uimara wa Ukawa ulioleta upinzani mkali lakini anaamini kwa utendaji wake wa kazi ni dhahiri kuwa ushindi huo utapanda kwenye uchaguzi wa mwaka 2020.

“Hakuna haja ya kupiga ramli, mambo anayofanya yanaweza kubadili upepo, ingawa inapaswa kueleweka kuwa CCM ni chama cha siasa kinachoshiriki uchaguzi kama vyama vingine vya siasa, ingawa dhamira yetu ni  kushinda kama ilivyo dhamira ya vyama vingine,” Mzee Msekwa alikaririwa.

Mwanasiasa huyo mkongwe alisisitiza kuwa CCM iko imara hivi sasa na imeendelea kuwa na umoja tofauti na inavyoelezwa na baadhi ya watu kuwa chama hicho kimepasuka.

 

Picha: Dk. Slaa afunga pingu za maisha na Josephine Mushumbusi
Malinzi aubariki ushindi wa Rais mpya wa FIFA, ampongeza