Kocha Mkuu wa Plateau United, Abdul Maikaba, ameonesha matumaini ya kulipiza kisasi na kuiondoa Simba SC kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, watakaporudiana siku ya Jumamosi (Desemba 05) Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Maikaba ameonesha matumaini hayo alipozungumza na waandishi wa habari dakika chache kabla ya kuanza safari ya kuja nchini Tanzania, tayari kwa mchezo huo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka wa Dar es salaam na kwingineko.

Kocha huyo amesema kwa hakika mchezo utakua na upinzani wa hali ya juu, lakini amejiandaa kukabiliana nao, hasa baada ya kuwafahamu vizuri Simba SC ambao amedai wana kikosi kizuri.

“Ulikua mchezo mzuri sana, nimewafahamu vilivyo Simba SC, nimetambua mapungufu yao, nitayafanyia kazi kabla ya mchezo wa mkondo wa pili ambao tutacheza Jumamosi,”

“Ninaamini bado kikosi changu kina kila sababu ya kupata ushindi dhidi ya wapinzani wetu, haijalishi itakua ugenini ama wapi, kama wao walishinda hapa kwetu, kwa nini sisi tusishinde kwao?” amehoji Maikaba.

“Niwaombe mashabiki wa soka hapa Nigeria waendelee kuwa na imani na Plateau United, binafsi sina shida na hilo kwa sababu tunakwenda kupambana, na In Shaa Allah tutapata matokeo mazuri.” Ameongeza kocha Maikaba.

Plateau United itahitaji ushindi wa mabao 2-0 ama zaidi ili kusonga mbele wakati timu hizo zitakaporudiana Jumamosi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam majira ya saa 11 jioni, wakati Simba yenyewe itakuwa ikihitaji sare ya aina yoyote au ushindi.

Mshindi wa jumla kati ya Simba na Plateua United, atakutana na Costa do Sol ya Msumbuji ama FC Platinum ya Zimbabwe ambayo katika mechi ya awali nayo ilishinda kwa mabao 2-1 ugenini.

Bobi Wine asitisha kampeni
Barr: Hakuna ushahidi wa madai ya wizi wa kura Marekani

Comments

comments