Kocha Mkuu wa Singida Big Stars, Hans Pluijm amesema atahakikisha kikosi chake hafanyi makosa hata kidogo, katika michezo miwili mfululizo itakayowakutanisha na Young Africans kwenye Uwanja wa CCM Liti mkoani Singida.
Singida Big Stars itaanza kucheza na Young Africans Mei 4, mchezo wa Ligi Kuu, kabla ya kucheza tena na mabingwa hao Mei 7, katika mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.
Kocha Pluijm amesema anafahamu Young Africans wana umahiri mkubwa kwenye kutumia nafasi wanazozipata, hivyo anakiandaa kikosi chake kukabiliana na hali hiyo, na ikiwezekana kuvuruga mipango yao ndani ya dakika 90.
Kocha huyo kutoka Uholanzi amekuwa akiifatilia Young Africans kwenye michezo ambayo inacheza na kuona wapinzani wake wamekuwa wazuri kwenye kutumia makosa na kupata ushindi.
“Tupo kwenye Nusu Fainali na tutacheza dhidi ya Young Africans, kwenye mpira kila kitu kinawezekana na hakuna kinachoshindikana pale ambapo utakuwa unaamini kwamba unaweza kufanya,”amesema Pluijm
Mchezo wa Mzunguuko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Africans uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Singida Big Stars iliambulia kichapo cha 4-0.