Kocha Mkuu wa Singida Fountain Gate FC, Hans Van der Pluijm, amesema michuano ya Ngao ya Jamii imemsaidia kuimarisha kikosi chake kuelekea michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo watashiriki msimu huu 2023/24.
Singida Fountain Gate imemaliza katika nafasi ya nne baada ya kupoteza mechi ya mshindi wa tatu waliyocheza dhidi ya Azam FC.
Kikosi cha timu hiyo tayari kimerejea Dar es Salaam ili kujiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya JKU ya Zanzibar utakaopigwa Agosti 18, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex na marudiano juma moja baadae.
Pluijm amesema malengo yao yalikuwa ni kutwaa taji hilo lililochukuliwa na Simba SC lakini mechi mbili walizocheza zimewasaidia wachezaji wake kuimarika zaidi.
Pluijm amesema amepata mwanga wa kuona madhaifu yao ikiwamo safu ya ushambuliaji na ulinzi ambayo ilikuwa na makosa katika mechi dhidi ya Azam FC ambayo walifungwa mabao 2-0.
“Hatukufikia malengo yetu lakini ni michezo imetusaidia kuandaa kikosi kuelekea mechi yetu ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, haitakuwa mechi rahisi kwa sababu wapinzani wetu wamejipanga vizuri.
“Hayo mashindano sio rahisi kwa sababu timu zilizofanikiwa kucheza michuano hii walifanya vizuri katika ligi zao, hatutawadharau kwa sababu tunahitaji kusonga mbele katika michuano hiyo,” Pluijm amesema.
Singida Fountain Gate yenyewe itaanza kampeni ya kuwania taji la Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuwakaribisha Tanzania Prisons Agosti 22, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Liti, mkoani Singida.
Pazia la Ligi Kuu Bara litafunguliwa rasmi leo Jumanne (Agosti 15) kwa Ihefu FC kuwakaribisha Geita Gold FC wakati Dodoma Jiji itawaalika Coastal Union na JKT Tanzania itawafuata Namungo FC mkoani Lindi.