Baada ya uongozi wa klabu ya Borussia Dortmund kufanya maamuzi ya kumtimua meneja Lucian Favre, aliyekua meneja wa Tottenham Hotspurs Mauricio Pochettino anatajwa huenda akarithi mikoba ndani ya klabu hiyo ya Ujerumani.
Favre alitimuliwa baada ya Dortimund kupata kichapo cha aibu cha mabao 5-1 dhidi ya VfB Stuttgart mwishoni mwa juma lililopita, huku wakipoteza mchezo wa tatu kwenye Ligi ya Ujerumani.
Pochettino ambaye kwa sasa hana kazi, baada ya kuondoka Spurs msimu uliopita, jina lake ni sehemu ya majina ya mameneja wanaoendelea kujadiliwa na viongozi wa Borussia Dortmund.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa, viongozi wamejizatiti kuwa na meneja ambaye ataweza kwenda sambamba na misingi iliyoachwa na Jurgen Klopp.
Mameneja wengine waliopo kwenye orodha inayojadiliwa na viongozi wa Borusia Dortimund ni Marco Rose wa Borussia Monchengladbach na Jesse Marsch wa RB Salzburg.