Kiungo Paul Pogba huenda akaihama Man utd katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi, na kutimkia kwa mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona.
Pogba ambaye ni miongoni mwa wachezaji walioiwezesha timu ya taifa ya Ufaransa kutwaa ubingwa wa dunia mwezi Julai mwaka huu nchini Urusi, ameonyesha kuwa tayari kuihama Man Utd, baada ya kuwaambia wachezaji wenzake wa klabu hiyo kuwa anataka kuondoka Old Trafford.
Kiungo huyo alifikisha ujumbe huo kwa jamaa zake huko Old Trafford baada ya kurejea kambini akitokea mapumzikoni, na naamini suala hilo litakamilishwa kabla ya dirisha la usajili halijafungwa rasmi barani Ulaya mwishoni mwa mwezi huu.
Mbali na kufikisha ujumbe kwa wachezaji, pia inadaiwa Pogba mwenye umri wa miaka 25, amefanya hivyo kwa mtendaji mkuu wa Man Utd Ed Woodward.
Hata hivyo msimamo wa klabu unaonyesha wazi, mchezaji huyo hatoingizwa sokoni kama anavyohitaji, na badala yake ataendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Jose Mourinho ambacho siku ya Ijumaa kitaanza kampeni ya kusaka ubingwa wa England msimu wa 2018/19, kwa kucheza dhidi ya Leicester City.
Dhumuni kubwa la mchezaji huyo kutaka kuihama Man Utd, ni kuhitaji uhuru wa kucheza kama ilivyokua zamani akiwa na Juventus FC, tofauti na sasa ambapo mara kadhaa amekua akionyesha kutoridhishwa na mfumo wa Jose Mourinho.
Vyombo vya habari nchini Hispania vinaeleza kuwa, endapo Pobga atafanikisha kujiunga na FC Barcelona atasaini mkataba wa miaka mitano utakaomuwezesha kulipwa mshahara wa Pauni 346,000 kwa juma, huku ada ya uhamisho wake inatajwa kufikia Pauni milioni 89.5.
Alipoulizwa wakala wa mchezaji huo Mino Raiola kuhusu ukweli wa jambo hilo alisema: “Sitojibu lolote kuhusu Pogba, muulizemi mwenyewe ama viongozi wa Man Utd.”