Kocha Gary Neville amesema kuwa anaamini mchezaji wa Manchester United, Paul Pogba hivi sasa hataki kuwa ndani ya klabu hiyo hasa baada ya kushawishiwa na wakala wake, Mino Raiola.
Pogba anahusishwa na taarifa za kutaka kutimkia Real Madrid, lakini Neville anaamini akili yake tayari imeshageuka.
Neville ambaye aliwahi kuichezea timu hiyo kwa muda mrefu zaidi wa maisha yake ya soka, amedai kuwa hata uchezaji wa Pogba anapokuwa uwanjani unaonesha dhahiri kuwa hana mapenzi aliyokuwa nayo awali kwa wekundu hao wa Old Trafford.
“Nadhani hataki kuwa hapa, hilo ndilo tatizo. Nadhani wakala wake amefanikiwa kumuingia,” alisema Neville.
“Nilisema miezi miwili, miezi mitatu iliyopita wakati huo alikuwa vizuri, alifanya vizuri sana kwa Ole, alifunga nadhani magoli 11 na kusaidia magoli saba,
“Lakini sasa… tunamjua wakala wake, tunafahamu jinsi alivyo na ushawishi kwake, tunajua kuwa Pogba ameshageuzwa kichwa na timu nyingine na anacheza kama mtu ambaye kichwa chake na akili vimeshageuzwa,” Neville aliiambia Sky Sports.
Pogba ana mkataba wa kuitumikia United hadi mwaka 2021 na pia unatoa nafasi ya kuongeza kipindi cha miezi mingine 12.
Kiwango chake kimeonekana kuwatia shaka wadau wa timu hiyo, hususan kutokana na jinsi ambavyo imepoteza matumaini ya kumaliza katika nafasi nne za juu kwenye Ligi.
Kwa kiasi kikubwa, lawama za kuporomoka kwa timu hiyo zinaelekezwa kwa Ole Gunnar Solskjær aliyepokea kijiti kutoka kwa Jose Mourinho. Solskjær alianza na ushindi mfululizo lakini mambo yamebadilika na amejikuta akipipigwa mfululizo.