Saa chache baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad kuhamia ACT-Wazalendo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amesema kuwa alichokifanya mwanasiasa huyo ni fundisho kuhusu siasa na utawala bora nchini.
Amesema kuwa mchakato wa mwanasiasa huyo kuhama chama na maamuzi ya mahakama vinatoa picha ya wazi kuwa kuna utawala bora nchini na kwamba watu wana haki ya kufanya siasa kwa uhuru.
“Utawala wa sheria unautaka Muhimili wa Mahakama kufanya kazi bila kuingiliwa, watu wanazo haki za kufanya uamuzi wa kisiasa na kujiunga na chama chochote,” Polepole anakaririwa.
“Hili ni fundisho kwa wale wote wanaosema kwamba mtu kujiunga na chama… hii imedhihirisha ni uhuru wao wa kisiasa,” Mwananchi linamkariri.
Maalim Seif ambaye ni miongoni mwa wanasiasa walioijenga CUF hususan visiwani Zanzibar alitangaza kujiunga na ACT Wazalendo jana, saa chache baada ya Mahakama Kuu kuhalalisha uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa wa kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti wa chama hicho.
Profesa Lipumba ambaye amekuwa kwenye mgogoro mkubwa na Maalim tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 alichaguliwa tena wiki iliyopita na Mkutano Mkuu wa chama hicho kuwa mwenyekiti. Mwanasiasa huyo ambaye pia ni mwanazuoni alimuondoa rasmi Maalim Seif kwenye nafasi ya ukatibu mkuu.