Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amewanyooshea kidole wajumbe wa Kamati ya Siasa wa Kata ya Kidatu mkoani Morogoro waliojiuzulu nafasi zao akieleza kuwa wamekisababishia hasara chama hicho.
Wajumbe hao walijiuzulu nafasi zao za uongozi wakiongozwa na mwenyekiti wa kamati hiyo, Magungu Alex wakati mchakato wa uchaguzi wa ndani wa chama hicho ukiendelea. Viongozi hao walikuwa wamebakiza miezi michache kukamilisha muhula wao wa uongozi.
Katika taarifa yake, Polepole ambaye anaendelea na ziara ya kuimarisha chama hicho tawala alisema kuwa viongozi hao wameisababishia harasa CCM kwani walishindwa kutekeleza majukumu yao kwa muda wa miaka mitano huku wakituhumiwa kwa usaliti katika uchaguzi wa mwaka 2015.
“Wamekisababishia chama hasara kwa miaka mitano yote walipokuwa madarakani, kwa sasa sioni kama wamejiuzulu ila muda wao umekwisha,” alisema Polepole.
Aidha, Polepole alisema kuwa CCM haipaswi kugeuzwa kuwa chama cha viongozi kwani msingi wa chama hicho ni kuwa chama cha wanachama wote kinachoshughulikia shida za wananchi.
CCM inaendelea na mchakato wa uchaguzi wa ndani wenye lengo la kuwapata viongozi wapya wa ngazi zote watakaokaa madarakani kwa muda wa miaka mitano.