Balozi na Mkuu wa Kituo cha Uwakilishi – Havana Nchini Cuba, Humphrey Hesron Polepole amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Mhe. Miguel Díaz-Canel Bermúdez Rais wa Jamhuri ya Cuba.
Baada ya kuwasilisha hati hizo, Balozi Polepole amekuwa na mazungumzo mafupi ambapo amempa salamu za mshikamano kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Naye Rais Díaz-Canel amemhakikishia ushirikiano mkubwa na ambao umejengwa katika misingi imara na waasisi Mwalimu Julius Nyerere Rais wa kwanza wa Tanzania na Kamanda Fidel Castro Kiongozi wa Mapinduzi ya Cuba.
Pia Balozi Polepole amekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Wizara ya Elimu ya Cuba ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya siku ya kimataifa ya Kiswahili itakayoadhimishwa tarehe 7 Julai 2023 ambapo uongozi wa Wizara ya Elimu ya Cuba umeridhia kuwa sehemu ya Maandalizi ya maadhimisho hayo.