Baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kueleza uchambuzi walioufanya kuhusu hali ya uchumi nchini uliotokana na vikao vya Kamati Kuu ya chama hicho kupitia ripoti ya Benki Kuu (BoT), Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole amejibu akizipita kando.
Akitoa tamko la chama hicho kufuatia kikao cha Kamati Kuu, Mbowe alisema kuwa wamefuatilia na kuchambua ripoti ya uchumi ya BoT inayotolewa kila mwezi na kubaini kuwa hali ya uchumi inazorota ukilinganisha na awamu iliyopita.
Akisoma taarifa yake kwa waandishi wa habari, Mbowe alisema kuwa hali ya uchumi imeshuka akigusia kuwa sekta ya Kilimo ambayo inategemewa na asilimia 75 ya Watanzania imekuwa kwa asilimia 1.7 pekee mwaka 2016/17, kiwango ambacho alidai kuwa ni cha chini kuwahi kutokea.
Aidha, Mbowe alisema kuwa hali ya fedha kwa wananchi imeshuka na hali ya ukata imeongezeka ukilinganisha na awamu iliyopita huku bei za vyakula kama mahindi na maharage ikipanda mara mbili ya ilivyokuwa miaka miwili iliyopita, kwa mujibu wa ripoti ya BoT.
Mbowe aliongeza kuwa hali ya mikopo kwa benki za biashara ni mbaya kiasi kwamba mikopo isiyolipika umevuka wastani wa asilimia tano hadi wastani wa asilimia nane na kusababisha baadhi ya benki kufungwa kutokana na hali hiyo. Chadema walidai pia kuwa deni la taifa limeongezeka, ambapo deni la ndani limeongezeka kwa zaidi ya dola bilioni 3,645.7.
Akizungumzia hoja hizo za Chadema, Polepole alizipita kando akieleza kuwa chama chake hakina muda wa kufanya malumbano kwani ina mkataba na wananchi kuwaletea maendeleo na sio vinginevyo.
“Sisi tuna mkataba na wananchi wa Tanzania kuhakikisha tunawaletea maendeleo. Kwa sasa tuko bize kufanya kazi hiyo. Kwakweli hatuna muda wa kufanya malumbano yasiyo na tija, tunachojua ni kazi kubwa iliyopo mbele yetu ambayo tumesaini mkataba mpaka mwaka 2020,” Polepole anakaririwa na Mwananchi.
Katika hatua nyingine, Msemaji wa Serikali, Dk. Hassan Abbas alisema kuwa hoja za uchambuzi wa Chadema hauendani na hali halisi ya miradi ya maendeleo inayoendelea kote nchini.
“Serikali inaajiri wafanyakazi wapya, inalipa mishahara kwa wakati, miradi ya maji inaendelea nchi nzima ikiwemo mikubwa ya kutoa maji Ziwa Victoria. Wanataka ushahidi upi zaidi ya ushahidi huu kuwa uchumi wa nchi unawafaidisha wananchi kupitia huduma hizo,” Dk. Abbas alihoji.
Dk. Abbas aliwataka Chadema kuangalia miradi mikubwa ya ujenzi inayoendelea nchi nzima na huduma ya afya kama ununuzi wa dawa na kwamba hata wabunge wa chama hicho hulipwa posho zao kama kawaida wawapo bungeni.