Mbunge wa Kuteuliwa na Mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi Humphrey Polepole amekanusha taarifa za kutaka kuhama chama cha mapinduzi na kuunda chama kipya alipozungumza katika mahojiano maalumu na kituo cha Habari cha Dar24
Polepole ametoa kauli hiyo alipoulizwa swali endapo atafutwa uanachama kutokana na kuendelea kuwa na tuhuma ndani ya CCM na kuendelea kuhojiwa, na amesema anaamini Chama Cha Mapinduzi kina utaratibu mzuri wa kujali haki za mwanachama
“Mi sio mbashiri na siwezi kubashiri kwa sasa na itakapofika hukumu ya chama nitazungumza wakati huo, na ni mazingira ambayo tunaamini yanaweza kutokea lakini hayatokei” Amesema Polepole
Polepole amesema hana mpango wowote wa kwenda chama kingine na kuondoka CCM kwa sababu alijiunga na chama hicho kwa hiyari na alifanya uchambuzi na kutazama historia ya vyama vyote akiamini itikadi za CCM za ujamaa na kujitegemea zinafaa kuwahudumia wananchi
“mimi kama nilijiunga kwa hiyari na CCM ninasema sitaondoka kwa Hiyari kwenye CCM naliweka wazi kwa watu wote wanaodhani eti mi naweza nikaondoka wapi we bwana weee” Alisisitiza Polepole
Wakati huo huo Polepole amesema hakuanza kufanya majukwaa ya kisiasa mitandaoni kwa kuwa alikasirika kuondolewa nafasi ya uenezi bali aliamua mwenyewe ni njia ipi inamfaa
“Sijaondolewa kwenye nafasi ya uenezi, na napenda kuwatangazia umma wa Tanzania kuwa nilishiriki katika kufanya mabadiliko ya katiba na kanuni ya chama inayosema kiongozi nafasi moja kofia moja, na nimeishi wakati wote kuhubiri kanuni hii, mimi ilipofika mwaka 2020 mamlaka ya urais iliamua kuniteua kuwa mbunge na nilitakiwa kuchagua kofia ipi nilipendelea na nilichagua Ubunge”
Hata hivyo Mbunge huyo amebainisha kuwa hatagombea tena Ubunge kwa sababu ya mazingira yake na miaka hii atakayokaa itamtosha kwa kuwa amewatumikia wananchi kwa kupitisha bajeti na ana amani tele kwa kuwa ameweza kupumzika kwa miaka baada ya harakati za uchaguzi wa mwaka 2020
Septemba 3, kamati ya maadili ya wabunge wa CCM ilimhoji Polepole kutokana na msimamo wake wa kupinga chanjo ya Uviko-19, huku msimamo wa Serikali na chama chake ukiwa ni kuhamasisha wananchi wapate chanjo hiyo.