Mbunge wa kuteuliwa, Humphrey Polepole, leo Jumanne Februari 9, 2021 amelieleza Bunge kuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli hana mpango wa kuongeza muda wa kukaa madarakani.
Polepole ambaye ni Katibu wa itikadi na uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), amesema ndani ya chama chao walishaelezwa hivyo na itabaki hivyo bila kubadilika.
Ametoa taarifa hiyo leo baada ya kuomba taarifa kufuatia kauli ya Mbunge wa Konde kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Khatibu Said Haji kumtaja Polepole kwamba alitumwa na Rais kusema juu ya kutogombea lakini amekaa kimya, kitendo ambacho kinawafanya Wabunge kuendelea kumtaka Rais Magufuli avunje Katiba wakati aliapa kuilinda.
“Nampongeza Rais Magufuli kwa uamuzi wake wa kuiheshimu katiba ya nchi hii, kabla yetu alitangulia kuapa, uamuzi wake wa kumtuma Polepole awaambie wana CCM kwamba hataongeza kipindi cha utawala ni ishara kwa kiongozi wetu kuilinda katiba.
“Mheshimiwa Polepole waambie CCM, Mheshimiwa Rais Magufuli hana shida ya kuongeza muda, alikutuma na video zinatembea tunaziona kwa nini unawaacha akina Sanga hapa wanaendelea kupotosha? Kwa nini hamheshimu mawazo ya Mheshimiwa rais?,” amehoji Khatib.
Baada ya hoja hiyo Polepole aliomba kutoa taarifa na kusema, “Naomba kumpa taarifa Mbunge kwamba masuala ya CCM yanazungumziwa kwenye vikao vya chama, hapa Bungeni wabunge wana uhuru wa kuzungumza lakini kinachozungumzwa hapa ndani hakiathiri msimamo wa chama tumekwishautoa rais hataongeza muda. Sisi ndani ya chama tulishaelezana na yeye (rais) ndiyo msemaji mkuu, lakini humu bungeni haizuii wao kutoa maoni yao.”
Katika michango ya Wabunge, Deo Sanga (Makambako) na Joseph Msukuma (Geita Vijijini) waliibua hoja iliyoanzia Bunge la 11 wakimtaka Rais Magufuli kufikiria namna ya kuongeza muda wa kuwa madarakani.
Hata hivyo, Polepole amesema hawezi kuzuia mijadala ya wabunge kwa kuwa ni haki yao kusema kile wanachokiamini ndani ya Bunge.