Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro amempandisha cheo askari polisi Meshack Samson wa Arusha aliyekataa kupokea rushwa ya Shilingi Milioni 10.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana amesema kuwa IGP Sirro amempandisha cheo Meshack kuwa Staff Sargent (Major). Kamanda Shana amesema kuwa mbali na kumpandisha cheo, IGP Sirro amemzawadia askari huyo Sh. 1 milioni.
Akieleza chanzo cha rushwa hiyo, amesema askari huyo alishawishiwa na watuhumiwa wawili kupokea kiasi hicho cha fedha ili aharibu ushahidi dhidi ya ndugu yao.
“IGP amempandisha cheo na kumzawadia shilingi milioni moja kwa kuwa mwadilifu na kutofuata mienendo mibaya ya baadhi ya askari wenzake,” alisema Kamanda Shana.
Kamanda Shana aliongeza kuwa askari IGP alimfuta kazi askari mwingine, Paul Edward (F8683) ambaye alikuwa anamshawishi Samson kuchukua rushwa hiyo.
Aidha, Kamanda Shana ameeleza kuwa Jeshi hilo pia limefunga kiwanda cha sukari kilichokuwa Njiro mkoani humo, kwa kufanya kazi bila kuwa na leseni na limeanza uchunguzi.