Katika tukio lisilo la kawaida, askari wa Jeshi la Polisi aliyetambulika kwa jina la Joel Francis ameripotiwa kumpiga hadi kumuua rafiki yake wa karibu aliyemtembelea nyumbani kwake.

Polisi huyo alimpiga hadi kumuua Donald Magalata mwenye umri wa miaka 30, kwa kutumia fimbo baada ya kubaini kuwa ‘wallet’ yake yenye pesa imepotea ndani ya nyumba hiyo na yeye¬†akashindwa kumpa majibu ya kumridhisha.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo amesema lilitokea katika siku ya Mwaka Mpya katika eneo la kambi ya polisi ya Mabatini wilayani Nyamagana.

“PC Joel alirudi kutoka kazini na alipofika nyumbani kwake alimkuta marehemu Magalata nyumbani kwake lakini alipobaini kuwa wallet yake haionekani ikiwa na kadi za benki (ATM Cards) na kitambulisho chake cha kazi, walianza kugombana,” alisema Kamanda Kamugisha.

Alisema kuwa Askari huyo alimfungia ndani marehemu na kumfunga pingu miguuni kabla hajaanza kumshushia kipigo kikali akidai wallet yake. Magalata alipiga kelele kubwa za kuomba msaada na ndipo majirani pamoja na polisi walipoingilia kati na kumkuta akiwa katika hali mbaya.

“Marehemu alikutwa akiwa amepoteza fahamu na kukimbizwa katika hospitali ya Bugando ambapo alipewa matibabu lakini alifariki siku iliyofuata,” alieleza.

Alieleza kuwa polisi wanamshikilia Francis kwa mahojiano zaidi.

Mugabe awavuruga Manabii wanaomtabiria Kifo
Polisi Wamkamata Kijana aliyejichora michoro ya ajabu na jina la Yesu