Askari Polisi anayefanya kazi ya ulinzi kwenye Bunge la Jamburi ya Kenya, Hellen Kwamboka amekutwa akiwa ameuawa nyumbani kwake jijini Nairobi, leo asubuhi.

Ripoti ya polisi imeeleza kuwa Kwamboka alikutwa amelala kitandani kwake akiwa na jeraha la kukatwa kwenye paji la uso. Damu inayotokana na majeraha hayo ilisambaa kwenye maeneo mbalimbali ya nyumba hiyo.

Imeelezwa kuwa mara ya mwisho, Kwamboka alionekana hadharani Alhamisi, Mei 23 alipokuwa anatoka kazini kuelekea nyumbani majira ya saa moja jioni.

“Alitakiwa kurejea kazini Ijumaa, Mei 24, lakini hakuonekana tena kazini,” imeeleza ripoti iliyotolewa kwenye kituo cha polisi cha Buruburu.

Polisi wameeleza kuwa marafiki wa Kwamboka walianza kumtafuta tangu Ijumaa, baada ya kushindwa kumpata kwenye namba zake za simu.

Mpenzi wa marehemu ndiye anayetajwa kuwa mtuhumiwa wa tukio hilo na polisi wameendelea kumtafuta. Polisi wanaamini kuwa kabla ya kifo chake kulikuwa na ugomvi na alipambana kabla ya kukatwa kwenye paji la uso.

“Hakuna silaha yoyote iliyokutwa kwenye eneo la tukio ambayo imechukuliwa na maafisa wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI),” imeeleza ripoti hiyo.

“Inaaminika kuwa mpenzi wake ambaye alimtembelea [Hellen Kwamboka], Mei 23, alimuua na kisha kutokomea. Simu za marehemu hazikuwa zinapatikana na inaonekana kama ziliibiwa na kuzimwa,” polisi wameeleza.

Mwili wa askari huyo ulipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika eneo la Chiromo na polisi wanaendelea kumsaka mpenzi wake.

Video: Sirro amhakikishia usalama Tundu Lissu, RC aamuru watumishi kusalimisha kadi za ATM, Lugola asimamisha wakuu wa polisi wilayani Geita
Hawa Maaskari wakamatwe, ni waharifu kabisa- Kangi Lugola

Comments

comments