Konstebo wa polisi nchini Uganda ameuawa na mtu ambaye anadaiwa kuwa na tatizo la akili baada ya kupigwa mawe hadi kufariki.
Akithibitisha kifo chake, Msemaji wa Polisi nchini humo Fred Enanga, alisema marehemu Francis Tindebwa, alikuwa akihudumu katika Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kyegegwa.
Enanga alisema kuwa Tindebwa alikutana na mauti yake wakati mwanaume mwenye ugonjwa wa akili alikwenda katika kituo cha polisi na kuanza kuwapiga mawe polisi waliokuwa zamu.
“Wakazi ambao wana matatizo ya kiakili wanapenda kufika kituoni. Mtu huyu alishtakiwa kidogo na alianza kusababisha shida katika kituo cha polisi. Alikuwa na tabia ya fujo na akaanza kuwapiga mawe maafisa wa polisi waliokuwa kazini,” Enanga alisema.
Kwa bahati mbaya Tindebwa aliyekuwa akisimamia kituo hicho alipatwa na jiwe hilo kwenye kichwa ambalo lilimpasua fuvu la kichwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Kyegegwa kabla ya kuhamishwa hadi Hospitali ya Kitaifa ya Mulago ambapo alithibitishwa kukata roho siku ya Jumapili, Februari 20.
Kwa mujibu wa Enanga hicho sio kisa cha kwanza kwa mgonjwa wa akili kumuua afisa wa polisi.
Enaga aliiomba wizara ya afya kujitokeza na kutafuta mbinu za kushughulikia suala la wagonjwa wa akili ambao alisema hivi sasa wamekuwa hatari kwa jamii.