Jeshi la Polisi nchini limesema halijazuia ibada za sikukuu ya Pasaka na kwamba walichozuia ni mikusanyiko, sherehe na makongamano ambayo yamekuwa yakifanyika katika sikukuu hiyo miaka ya nyuma.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Aprili 2, 2021 na Msemaji wa jeshi hilo, David Misime katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma.

Katika maelezo yake leo, Misime amesema taarifa inayosambaa katika mitandao ya kijamii kwamba polisi wamezuia ibada si ya kweli akisisitiza kuwa taarifa hizo zinalenga kupotosha umma na kuwachanganya waumini.

“Hata jana Alhamisi Kuu, Polisi wenye sare na waliovalia kiraia walikuwa kwenye doria kwa ajili ya kuimarisha ulinzi kwa wananchi ili wenye imani ya Kikristo waweze kwenda makanisani kuabudu kwa uhuru bila shaka,” amesema Misime.

“Ibada za Sherehe za Pasaka kwenye Makanisa, Sherehe za Kifamilia, Hitma, Familia kuungana na kwenda kutembelea sehemu mbalimbali na kusherehekea Pasaka hakuna aliyekataza ili mradi unachofanya kinaendana na kufuata utu, busara, hekima, Sheria , kanuni na taratibu za nchi,” amesema Kamanda Misime..

“Jambo ambalo hatutegemei kuliona ni zile shamrashamra kubwa kama vile Matamasha na Makongamano ya Pasaka na kwa bahati nzuri wanaoyaandaa kila mwaka kwa utu wao wa Kitanzania, hekima na busara zao hatujasikia wakitangaza maandalizi ya Matamasha hayo,” ameongeza Misime.

Jana Misime alitoa taarifa iliyoeleza kuwa polisi wamezuia shamrashamra za sikukuu hiyo kwa kuwa nchi ipo katika siku 21 za maombolezo ya kifo cha Rais wa awamu ya tano Hayati Dkt. John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021.

G7 yawashukia wanajeshi wa Eritrea
Akon atua Uganda