Jeshi la Polisi- Dar es salaam.

Jeshi la Polisi nchini, kupitia Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam – DPA, wameandaa mashindano ya Polisi Jamii, yatakayo shirikisha Wananchi na Askari wakilenga kushirikiana ili kutokomeza uhalifu na kuchangia Damu katika Benki ya Damu salama, zoezi ambalo litasimamiwa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke.

Mkuu wa Chuo hicho, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Dkt. Lazaro Mambosasa ameyasema hayo hii leo Agosti 15, 2023, Chuoni hapo na kudai kuwa ushirikishwaji wa Wananchi katika michezo hiyo itasaidia kubadilishana taarifa mbalimbali na Polisi zikiwemo za uhalifu na wahalifu.

Kwa upande wake Afisa Michezo wa chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam – DPA, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, SSP Salum Madongo amesema katika mashindano hayo wanatarajia kuhusisha michezo Kumi na Sita, ikiwemo mpira wa miguu kwa Wanaume na Wanawake, Mpira wa Wavu, Masumbwi, Taekwondo, Judo, riadha nk.

Naye Kocha wa Mpira wa Kikapu, Lincon Kagame, amesema wamefarijika kualikwa na kushiriki michezo ya Polisi Jamii ambapo amebainisha kuwa michezo hiyo itawaleta karibu na kuwaunganisha na jeshi la Polisi katika kupambana na uhalifu.

Mashindano hayo, yanatarajiwa kuzinduliwa Agosti 25, 2023 ambapo itakuwa siku ya ugawaji wa vifaa mbalimbali kwa timu zote shiriki, pamoja na zoezi la uchangiaji wa damu, na Septemba 4 mashindano yataanza rasmi na kumalizika Septemba 23, 2023.

Kakolanya aahidi balaa zito Singida FG
Elimu bora: Wanafunzi wa kike wawezeshe - Dkt. Tulia