Jeshi la Polisi mkoani Kigoma, limekamata silaha mbili za kivita pamoja na risasi 125 na kuuwa watu watano ambao wanasadikiwa kuwa ni majambazi.
Tukio hilo limetokea katika pori la Rusohoko lililopo Kibondo wilayani kasulu mkoani Kigoma ambapo majambazi walio uwawa pamoja na wengine waliotokomea kusikojulikana walikuwa wanajiandaa kutekeleza tukio la kuteka magari kwenye pori hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio Kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma, Martin Otieno amesema kuwa tukio hilo limetokea baada ya Polisi kumkamata jambazi mmoja akiwa anaenda kufanya uhalifu katika eneo hilo.
Baada ya kushukiwa, majambazi hao walianza kufyatua risasi na kujeruhi askari wawili, na katika majibizano hayo Polisi wakafanikiwa kuwapiga risasi majambazi watano ambao wamefariki dunia walipokuwa wanakimbizwa hospitali na wengine wakakimbia na kutokomea kusikojulikana.
Kamanda Otieno amesema katika tukio hilo wamefanikiwa kukamata bunduki mbili za kivita aina ya AK 47, magazine mbili na risasi 20 zilizokuwa zinatumika kwenywe uhalifu.
Katika hatua nyingine Polisi imemkamata mtu mmoja aitwae Oswald Zababa (48), mkazi wa kijiji cha Kagerankanda akiwa na risasi 105 za bunduki aina ya SMG na magazini moja.
Hata hivyo, Otieno amesema Polisi inaendelea na msako katika wilaya zote ili kuhakikisha wanatokomeza matukio ya ujambazi na yale ya utekaji, na kuwaomba wananchi kuendelea na shughuli zao kwa amani kwani Kigoma ni salama na Askari wapo barabarani muda wote.