Askari watatu wa jeshi la polisi nchini Kenya wamekamatwa kwa tuhuma za kumsaidia mtuhumiwa wa mauaji ya watu 10 anayefahamika kama Masten Millimo Wanjala, kutoroka selo.
Askari hao wametajwa kuwa ni Mpelelezi Philip Mbithi, Konstebo Boniface Mutuma na Precious Mwende, wote wa kituo cha polisi cha Jogoo jijini Nairobi.
Watatu hao wanakabiliwa na mashtaka ya kufanya uzembe, kula njama na kumsaidia mtuhumiwa kutoroka kinyume cha sheria ya makosa ya jinai.
Wanjala alikuwa anahusishwa na matukio ya kuwaua watu zaidi ya 10 na alikiri kufanya matukio hayo.
Inaelezwa kuwa afisa wa polisi aliyekuwa zamu alibaini Wanjala hayuko selo majira ya saa 1 asubuhi, Jumatano wiki hii, wakati alipaswa kupelekwa mahakamani siku hiyo akikabiliwa na mashtaka 13 ya mauaji.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Buruburu, Francis Kamau amesema kuwa Wanjala alitoweka kwenye mazingira ya kutatanisha, na kwamba huenda alitoroka wakati wa kupata chakula cha usiku kwakuwa siku hiyo kulikuwa na tatizo la umeme kuanzia saa 9 alasiri hadi saa 2 usiku.
Hata hivyo, siku moja baada ya taarifa za kutoroka kwake, Wanjala alikamatwa na watu wenye hasira katika kijiji cha Mukhweya eneo la Bungoma, ambao walimuua kwa kipigo.