Kikosi cha Maafande wa Jeshi la Polisi ‘POLISI TANZANIA’ kesho Jumatano (Oktoba 19) kitachezwa kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kama mwenyeji wa Uwanja huo, kuikabili Namungo FC kutoka mkoani Lindi.
Polisi Tanzania iliyokua inautumia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, imefikia maamuzi ya kuhamia jijini Mbeya ili kubadilisha mazingira ambayo wanaamini yanaweza kuwapa matokeo mazuri msimu huu.
Kocha msaidizi wa Polisi Tanzania Shadrack Nsajigwa amesema tayari kikosi kimeshawasili jijini Mbeya kwa ajili ya mchezo huo, ambao amekiri utakua mgumu na wenye changamoto nyingi za ushindani kutokana na uzuri wa kikosi cha wapinzani wao.
Amesema amefanya kazi kubwa ya kukiandaa kikosi cha Maafande hao ili kufanikisha mpango wa ushindi wao wa kwanza msimu huu, baada ya kuambulia vipigo vitano na kuambulia sare mbili.
“Mchezo utakua mgumu na ushindani mkubwa, tumefanya maandalizi mazuri kuhakikisha tunapata ushindi na kuendelea kujiweka katika mazingira mazuri katika msimamo wa Ligi Kuu.” amesema Nsajigwa
Wakati huo huo Uongozi wa Polisi Tanzania umeachana na Kocha kutoka nchini Burundi Joslin Sharif Bipfubusa, kufuatia matokeo mabovu yaliowaandama tangu mwanzoni mwa msimu huu 2022/23.
Kocha huyo amekiongoza kikosi cha Polisi Tanzania katika Michezo saba, akiambulia vipigo vitano na kutoka sare mara mbili, hali ambayo imeifanya timu ya maafande kuburuza mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu hadi sasa.