Benchi la Ufundi la Maafande wa Polisi (Polisi Tanzania) limetoa siri ya kumaliza msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa kupata alama 6 kwenye mchezo miwili iliyosalia.
Kocha Msaidizi wa maafande hao George Mketo, amesema ushirikiano ambao wanaonyesha wachezaji ndani ya uwanja unawapa nguvu ya kufanya vizuri kwenye michezo inayofuata kabla ya kufungwa kwa pazia la Ligi Kuu 2020/21.
Kocha huyo amesema kuwa kila mchezaji anatimiza majukumu yake ndani ya uwanja jambo ambalo linawafanya wawe na imani ya kupata matokeo kwenye mechi zao ambazo zimebaki.
“Kila mchezaji anapambana ili kupata pointi tatu ni lazima kila mmoja apambane ili kuona timu inashinda na kwa namna ambavyo wachezaji wanafanya kwetu ni furaha.
“Tunajua kwamba ushindani ni mkubwa hilo lipo wazi na ni jambo zuri kwa sababu ili kuwa na timu imara lazima ipate ushindani kutoka kwa wengine hilo halitupi tabu.”
Miongoni mwa wachezaji wakongwe ndani ya Polisi Tanzania ni pamoja na beki kisiki, Kelvin Yondan ambaye ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Malale Hamsini.
Yondani alijiunga na Polisi Tanzania akiwa ni mchezaji huru baada ya mabosi wake wa Yanga kuachana naye msimu uliopita.
Ikiwa imecheza jumla ya michezo 32 imekusanya alama 42 kwenye msimamo ipo nafasi ya 7 huku kinara akiwa ni Simba SC mwenye alama 73.