Umoja wa Mataifa, kupitia maafisa wake wanaohusika na usalama katika mkutano wa mazingira wa Umoja wa Mataifa COP27 nchini Misri, wanachunguza madai ya upelelezi na ukosefu wa maadili ya baadhi ya Polisi wa Misri, kwa washiriki wa mkutano huo.
Madai hayo ya upelelezi, yalizuka baada ya ujumbe wa Ujerumani kuandaa mkutano ambapo walimjumuisha Sanaa Seif, Dada wa mwanaharakati wa demokrasia. Alaa Abdel Fattah, ambaye yuko kifungoni na amegomea chakula.
Washiriki wa mkutano huo wa COP27, wakiwemo wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu na makundi ya kiraia, wamezungumzia visa vya kupelelezwa wakati wa mkutano huo, ulioanza Novemba 6, 2022 katika mji wa mapumziko wa Sharm El-Sheikh.
Awali, Shirika la kutetea haki za binadamu lililo na makao yake jijini New York, Human Rights Watch lililaani mpango wa Misri wa upelelezi, uliojumuisha kuwekwa kwa kamera za siri katika mamia ya usafiri wa magari ya kukodi mji wa Sharm El-Sheikh.