Mahakama Kuu nchini Kenya imewahukumu adhabu ya kifo, askari wawili wa jeshi la polisi baada ya kuwakuta na hatia ya mauaji ya watu watatu akiwemo mlinzi wa mbunge wa Bomachoge, Joel Onyancha.
Akisoma hukumu hiyo Jumatano wiki hii, Jaji S.N Mutuku alisema kuwa askari hao, Benjamin Kahindi Changawa na Stanley Okoti walimuua Joseph Obongo aliyekuwa askari anayemlinda mbunge huyo, pamoja na ndugu zake wawili katika eneo la Kangemi jijini Nairobi mwaka 2014.
Alisema kuwa askari hao walitekeleza mauaji hayo na kisha kusingizia kuwa watu hao walikuwa majambazi.
Ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo uliotumika kuwatia hatiani, ulitokana na uchunguzi uliofanywa na Kitengo cha Kujitegemea cha Uchunguzi wa Kipolisi (IPOA).
“Kufuatia mauaji hayo, IPOA ilianzisha uchunguzi Oktoba 7, 2014 kufahamu ukweli wa chanzo cha mauaji hayo, hususan kufahamu kama kulikuwa na sababu zozote za watuhumiwa kutumia risasi za moto,” ripoti ya IPOA ilisomwa mahakani hapo.
“IPOA ilihitimisha uchunguzi na kuwasilisha kwa Muendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) kuwa watuhumiwa wafunguliwe mashtaka ya mauaji. DPP alikubaliana na mapendekezo hayo baada ya kupitia vielelezo, na kufungua jarada rasmi Aprili 27, 2015,” iliongeza.
Imeelezwa kuwa marehemu walikuwa wakitembea kutoka katika bar moja ya eneo la Kangemi, wakielekea nyumbani kwao, usiku wa tukio hilo.