Mamlaka za usalama nchini Kenya, zimeahidi kukabiliana na uhalifu unaozidi kuota mizizi katika miji mbalimbali ikiwemo jiji la Nairobi baada ya wananchi wengi kuripoti ongezeko la visa vya uhalifu, na hasa majira ya mchana.
Mbele ya Waandishi wa Habari, Waziri wa mambo ya ndani wa Kenya, Kithure Kindiki amesema lipo kundi dogo la wahalifu waliojihami kwa visu na silaha nyengine na kuwahangaisha wakazi wa Nairobi na maeneo mbalimbali.
Amesema, jiji la Nairobi limekuwa likikumbwa na ongezeko la vitendo vya uhalifu na kusema wao kama chombo cha usalama watakabiliana na magenge ya vijana hao ili kurejesha amani miongoni mwa jamii.
Kwa upande wake, Inspekta Jenerali wa Polisi Kenya, Japhet Koome ametoa mwezi mmoja kwa yeyote anayemiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha silaha hizo la kabla ya upekuzi kuanza ili kuwabaini wahalifu wote.