Jeshi la Polisi Mkoani Arusha, kupitia operesheni mbalimbali dhidi ya madawa ya kulevya limefanikiwa kukamata Mirungi kilogramu 257.3, Bhangi kilogramu 98 pamoja na Heroine gramu 100 kwa kipindi cha kuanzia Julai 1, 2023.
Kamanda wa Polisi Mkoani humo, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo amesema mbali na madawa hayo pia wamefanikiwa kukamata watuhumiwa 32 wakiwa na pombe ya Moshi lita 238.5 na mitambo minne ya kutengeneza pombe hiyo.
Amesema pia wamefanikiwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa 28 wa makosa ya ukatili na baadhi yao wamehukumiwa kwenda jela vifungo mbalimbali ambapo kati ya waliohukumiwa, watuhumiwa watatu walihukumiwa kwenda jela vifungo vya maisha kwa makosa ya ubakaji na ulawiti na mtuhumiwa mmoja alihukumiwa jela miaka 30 kwa kosa la ubakaji.
Aidha, Kamanda Masejo amesema mafanikio hayo yametokana na elimu ambayo inaendelea kutolewa kwa wananchi ambao wamekua wakitoa ushirikiano kwa Jeshi hilo na kupelekea Mkoa huo kuendelea kuwa shwari hasa kwa kuzingatia ni kitovu cha Utalii Nchini.