Mwandishi wa Jeshi la Polisi

Jeshi la Polisi Kikosi cha Kupambana na Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini, katika kipindi cha mwezi Juni, 2023 wamefanikiwa kukamata mifugo 319 iliyokuwa imeibwa maeneo mbalimbali, na kuwakamata watuhumiwa 153 wa matukio tofauti ya wizi huo.

Akitoa taarifa hiyo hii leo Juni 16,2023 eneo la Kikatiti Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP. Simon Pasua amesema watuhumiwa hao tayari wamefikishwa Mahakamani na kesi zao zipo katika hatua mbalimbali.

Amesema, kikosi hicho kwa kushirikiana na wananchi wameunda vikundi vya ulinzi shirikishi, ili kutokomeza wizi wa mifugo na kubainisha kuwa wakaguzi kata waliopo katika maeneo mbalimbali nchini wameendelea kutoa elimu na kuwashauri wananchi kutowaacha watoto wadogo kuchunga mifugo.

Awali, baadhi ya wananchi akiwemo Wilson Shami wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa kupambana na uhalifu wa mifugo na kupelekea kupungua kwa wizi katika maeneo mbalimbali na kusema uwepo wa Askari Kata katika maeneo yao, umesadia kuweka nidhamu kwa walio na nia ya kuiba mifugo.

Kwa upande wake, Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Meru, Jobard Thadeo amelishukuru Jeshi la Polisi Kikosi cha Kupambana na Kuzuia Wizi wa Mifugo kwa jinsi linavyoshirikiana nao katika kutoa elimu juu ya kusimamia mifugo yao na kwamba uanzishwaji wa vikundi vya ulinzi, umesaidia kudhibiti uhalifu.

Hii hapa siri ya panga linaloendelea Azam FC
Mbappe hana lawama Paris Saint-Germain