Jeshi la Polisi mkoani Mara wilayani Tarime/Rorya limekamata mitambo minne ya kutengeneza pombe haramu (Gongo) mali ya Matinde Mbusiro (50) Pius Chacha (74), Chacha Mwera (47) na Mirumbe Makambi (61) wote wakazi wa Kijiji cha Nyansincha wilayani Tarime.
Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe ambapo amesema kuwa watu hao walikamatwa Juni, 25, 2019 majira ya saa 7 mchana pembezoni mwa mto Nkandare katika Kitongoji cha Kokimusi Kijiji cha Kobori.
Amesema kuwa siku hiyo majira ya saa 9 alasiri katika kitongoji cha Kokimusi Polisi walifanikiwa kukamata Pombe haramu lita 330 ikiwa imehifadhiwa ndani ya madumu ya plastiki rangi ya njano ikiwa imetunzwa kwenye nyumba ya Bwiru Keng’anya (20) na Ghati Keng’anya ((40) wote wakazi wa Kobori.
Kamanda Mwaibambe amewataka wananchi kutofanya biashara haramu na badala yake wafanye biashara halali ambazo hazitawaingiza kwenye matatizo na hivyo kutengana na familia zao baada ya kukamatwa kwa makosa mbalimbali kinyume cha sheria.