Kufuatia taarifa zinazosambaa mtandaoni kuwa gari ya mbunge wa viti maalumu mkoa wa Manyara (CHADEMA), Anna Gidarya limeshambuliwa kwa risasi, Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoani Manyara wote wamekanusha taarifa hizo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Manyara, Agustino Senga amesema amefuatilia lakini taarifa alizopata ni kwamba mbunge huyo hayupo Manyara yupo wilayani Monduli kwenye uchaguzi.

”Katika eneo langu nimefuatilia kwa watendaji wangu hakuna tukio hilo lakini nimeelezwa mbunge huyo yupo kwenye mambo ya uchaguzi huko Monduli labda uwasiliane na kamanda wa Arusha”, amesema Kamanda Senga.

Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha (SACP) Ramadhani Ng’anzi amesema hana taarifa juu ya tukio hilo huku akieleza mpaka sasa hali ni shwari katika uchaguzi wa Monduli.

”Tukio hilo sijalipata huku kwangu maana uchaguzi unaendelea vizuri watu ni wengi, usalama ni wa kutosha labda kama itabainika hivyo nitatoa taarifa lakini kwasasa sina taarifa hiyo”, amesema Kamanda Ng’azi.

Taarifa inayosambaa mtandaoni inaeleza kuwa gari la mbunge huyo limeshambuliwa kwa risasi tairi zake. Endelea kuwa nasi muda wote tutaendelea kukufahamisha undani wa tukio hili kadri tunavyopata taaarifa.

 

 

NEC yaelezea kuhusu Mawakala waliokatatiliwa
Video: Mgombea ajiuzulu dakika chache kabla ya uchaguzi