Jeshi la polisi nchini Afrika Kusini leo limetumia risasi za mipira na gesi pamoja na maji ya kuwasha kuwatawanya waandamanaji wanaopinga wahamiaji na wageni, jijini Pretoria.
Tangu wiki iliyopita, makundi makubwa ya waandamanaji hao ambao wanaripotiwa kuwa na silaha za jadi kama visu, mawe na fimbo limekuwa likivamia maduka ya wahamiaji na wageni wakivunja na kuwashambulia wamiliki, kwa kile wanachodai kuwa wamechukua kazi na fursa za wazawa.
Kwa mujibu wa BBC, chopa ya polisi ilitumika kutawanya makundi mawii ya waandamanaji, wanaopinga wageni na wale ambao wanaunga mkono uwepo wa wageni. Makundi hayo yote yameripotiwa kutumia silaha za jadi.
Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma amewataka wananchi wote kuwa watulivu wakati vyombo vya dola vikiendelea kushughulikia hali ya usalama. Mkuu huyo wa nchi amelaani vikali vitendo vinavyofanywa na waandamanaji wanaowapinga wageni.
Zuma amesema kuwa wahamiaji wengi na wageni kutoka nchi mbalimbali wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo.
“Ni kosa kuwachukulia watu wote ambao sio raia wa nchi hii kama wafanyabiashara wa dawa za kulevya au wafanyabiashara haramu ya binadamu. Tuwatenge wote ambao wanafanya kosa hilo na tushirikiane na Serikali kuwatia nguvuni bila ubaguzi na bila kufanya madhara kwa wananchi wasio na hatia,” alisema Rais Zuma.
Alisisitiza kuwa ataongoza vita dhidi ya uhalifu huo kuhuisha jamii iliyo salama na imara.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo amesema kuwa wanaendelea na mchakato wa kutembelea maeneo yote ya kazi kufanya ukaguzi ili kubaini kama kuna raia wa kigeni wanaofanya kazi bila kuwa na vibali maalum.