Jeshi la Polisi nchini limemkamata Wilfred Masawe (36), mkazi wa Buza, Temeke jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za utapeli kwa njia ya mitandao.

Mtuhumiwa huyo amedaiwa kutumia mbinu mbalimbali kutapeli zikiwemo kujitambulisha kama kiongozi wa Serikali kwa kutumia mtandao wa Whatsapp, huku akieleza kuwa yuko nje ya nchi na kwamba kuna tatizo la msiba ambao umetokea nchini na unamhusu. Hivyo, alikua akitoa maelekezo kwa watendaji wa Serikali waweze kusaidia gharama za matibabu hospitalini, gharama za kusafirisha mwili wa marehemu na gharama za mazishi.

Pia, mtuhumiwa huyo alijifanya kuwa Askofu wa kanisa moja la Kikristo. Alitumia cheo hicho cha kugushi kuwalaghai waumini na viongozi mbalimbali akidai kuandaa makongamano makubwa ya kidini, lengo likiwa kuwachangisha fedha kwa kigezo cha kutaka kufanikisha makongamano hayo.

“Baadhi ya matukio aliyofanikiwa kutapeli ni pamoja na viongozi wa dini, viongozi wa Serikali, wafanyabiashara, mameneja na wakurugenzi wa taasisi za umma, wanasiasa pamoja na waumini wa madhehebu ya dini,” Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba anakaririwa.

Bulimba alieleza kuwa mtuhumiwa huyo alitekeleza matukio hayo peke yake kwa njia ya maandishi (SMS na WhatsApp) bila kuzungumza na mtu aliyemlenga kwa njia ya simu.

Video: Lema aanza kuuona moshi mweupe, Mabaki ya Faru John utata mtupu...
Video: Maneno ya Naibu Waziri Anastazia Wambura kuhusu sanaa Tanzania