Jeshi la Polisi Tanzania, limemuaga rasmi IGP Mstaafu, Balozi Simon Nyakoro Sirro hii leo Jumatano Mei 10, 2023 baada ya kustaafu Utumishi ndani ya Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria Machi 2023.
Sherehe za kumuaga Sirro zimefanyika Chuo cha Taaluma ya Polisi Dares Salaam – DPA, kilichopo Kurasini Jijini Dar es Salaam kwa gwaride maalum kama utaratibu wa Jeshi unavyoelekeza wa gwaride maalum Viongozi wa Polisi waliofikia cheo cha Kamishna wa Polisi na Inspekta Jenerali wa Polisi.
IGP Mstaafu, Balozi Simon Nyakoro Sirro amelitumika Jeshi la Polisi kwa miaka 30 tangu Februari 19, 1993 alipojiunga rasmi hadi kustaafu mwezi Machi, 2023 akiwa ni Mkuu wa Jeshi la Polisi wa 10 tangu uhuru wa 1961 akiongoza kuanzia Mei 28, 2017 hadi tarehe 20 Julai 2022.
Wengine waliowahi kushika nyadhifa hiyo ni ya ukuu wa Jeshi la Polisi ni IGP Mstaafu wa kwanza nchini, Elangwa Shaidi (1964 -1970), Hamza Azizi (1970 – 1973), Samweli Pundugu (1973- 1975), Philemon Maya (1975-1980), Solomon Liani (1980 – 1984), Harun Mahundi (1984-1996) Omari Mahita (1996 – 2006), Saidi Mwema (2006-2013) na IGP Mstaafu Ernest Mangu (2013-2017).