Askari wa Jeshi la Polisi nchini Zimbabwe wamepigwa marufuku kula chakula hadharani pamoja na kuvuta sigara hadharani.
Uamuzi huo umetolewa na Jenerali Godwin Matanga aliyeteuliwa hivi karibuni, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kusafisha taswira ya jeshi hilo wakati nchi hiyo ikielekea katika uchaguzi mkuu.
Kwa mujibu wa gazeti linalomilikiwa na Serikali la Herald, Matanga pia alipiga marufuku askari polisi kutembea wakiwa wameweka mikono yao mifukoni.
Alisema kuwa askari wa jeshi la polisi wanatakiwa kuhakikisha wanavaa sare za jeshi hilo ili waonekane zaidi na kuacha kutumia muda wao katika mitandao ya kijamii au simu za mkononi wakati wa kazi.
Akiwahutubia viongozi waandamizi wa jeshi hilo wiki iliyopita jijini Harare, Jenerali Matanga alionya polisi kutojihusisha na vitendo vya rushwa na kuhakikisha wanakuwa watiifu.
Bosi huyo wa Jeshi la Polisi ametoa kauli hizo siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Obert Mpofu kusaini makubaliano ya hiari ya kujiunga na nchi ya Belarus kwa lengo la kufanya mageuzi katika jeshi la nchi hiyo.
Mwaka jana, Belarus ilitajwa kuwa miongoni mwa nchi kumi zenye kiwango kidogo cha uhalifu na usalama wa hali ya juu.
Waziri Mpofu alisema kuwa Belarus itasaidia nchi hiyo kuliunda upya jeshi la polisi kuwa jeshi la kutoa huduma kufuatia kupoteza imani kwa wananchi kwa tuhuma za rushwa.
Alisema nchi hizo pia zitasaidiana kupambana na uhalifu, madawa ya kulevya pamoja na ugaidi.