Mahakama nchini Kenya imewafunga jela askari wawili wa jeshi la polisi baada ya kuwakuta na hatia ya kumuua mfanyabiashara wa kike katika eneo la City Park, Nairobi.

Katika uamuzi huo wa Mahamaka, imeelezwa kuwa askari hao waliotambulishwa kwa jina la William Chirchir na Godfrey Kirui walifanya kosa hilo mwaka 2018.

Imeelezwa kuwa Mei 20, 2018 askari hao wawili walifyatua risasi kuelekea kwenye gari alilokuwemo Janet Waiyaki na binamu yake, Bernard Chege na kusababisha kifo cha mwanamke huyo.

Mahakama imewakuta wawili hao na hatia ya kuua bila kukusudia ikilieza kuwa nguvu waliyotumia haikuwa inaendana na hatari iliyokuwa mbele yao.

Jaji wa Mahakama Kuu, Stella Mutuku Ushahidi uliwasilishwa mahakamani hapo umeonesha kuwa hakukuwa na kosa lolote lililofanywa na marehemu au binamu yake huyo. 

Jaji huyo alieleza kuwa askari hao walifyatua risasi bila kutambua watu waliokuwa kwenye gari hilo walipokuwa wanaondoa gari lao. Amefafanua kuwa risasi hizo zilielekezwa moja kwa moja kwenye viti vya gari walivyokalia na sio hewani kama walivyodai.

“Walifanya tabia ya ajabu na ya haraka, walifyatua risasi kwa lengo la kuua,” alisema Jaji Mutuku, akifafanua kuwa walitumia vitisho na silaha kuisimamisha gari hilo.

“Maafisa hawa wa polisi walikuwa na silaha za moto, walipaswa kufanya vitendo vyote kwa uangalifu. Ninaamini kuna njia nyingine bora ambazo wangetumia, na pia walipaswa kuzingatia sheria kulinda maisha ya watu,” aliongeza.

Mfanyabiashara huyo aliyekuwa na umri wa miaka 41 alifariki na binamu yake mwenye umri wa miaka 26 alijeruhiwa vibaya kwa risasi.

Ndumbaro apokea taarifa ya ubadhirifu TTB
Meya aagiza kusitishwa ununuzi wa bastola ya Mkurugenzi