Jeshi la Polisi limelishukia kundi la ucheshi la ‘Original Comedy’ kwa kuvaa mavazi yanayofanana na sare za jeshi hilo kwenye harusi ya Emmanuel maarufu kama ‘Masanja Mkandamizaji’.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, ACP Advera John Bulimba kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari ameeleza kuwa Jeshi hilo litawachukulia hatua za kisheria wachekeshaji hao kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

“Kwa mujibu wa Sheria ya kanuni za makosa ya Jinai, sura ya 16 na  marejeo yake ya mwaka 2002,  kifungu cha 178 (1) na  (2) kinachozungumzia makosa dhidi ya sare za majeshi ya ulinzi na usalama,  kinabainisha wazi kuwa ni kosa kisheria kwa mtu yeyote ambaye siyo mtumishi wa majeshi ya ulinzi na usalama kuvaa mavazi yanayotumiwa au kushabihiana na sare za majeshi hayo  bila kibali kutoka kwa  Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” inaeleza taarifa ya ACP Advera.

Aidha, alitoa onyo kwa watu wanaovalia mavazi yenye mfanano wa sare za majeshi yote nchini akieleza kuwa watakaobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Aliwataka wale wote wanaomiliki mavazi ya aina hiyo kuyasalimisha mara moja katika vituo vya polisi vilivyo katika maeneo yao.

Waigizaji wa kundi la Original Comedy walifunikwa kwa uchezi wa aina yake katika harusi ya mwenzao iliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, huku wakiwa wamevalia mavazi yanayofanana na sare za jeshi la polisi.

 

Mkurugenzi amwaga machozi mbele ya Kamati ya Bunge
Video: Makonda aweka wazi jambo hili, Atoa maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya