Jeshi la polisi nchini Afrika Kusini limewaua kwa risasi kanisani watu saba wanaotuhumiwa kuwaua askari polisi.
Taarifa ya polisi imeeleza kuwa watu hao waliopigwa risasi kanisani walikuwa wanatafutwa kwa kuwaua askari wa jeshi hilo Jumatano wiki hii katika kituo cha polisi kilichoko Cape Town.
Aidha, imeeleza kuwa katika harakati hizo za mashambulizi, watu kumi wengine wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji hayo walikamatwa katika kanisa moja kwenye kijiji cha Nyanga huku baadhi wakitoroka.
Kamishna wa Polisi wa Afrika Kusini, Khehla Sitole aliuambia umati uliokuwa umekusanyika nje ya kanisa kuwa jeshi hilo limejipanga kuhakikisha watu wote waliohusika na mauaji hayo wanafikishwa kwenye mikono ya sheria na kwamba wengi walikuwa wanajificha kanisani.
“Tumeamua kwamba hali hii haitaendelea kufanyika hapa Afrika Kusini kwa uhalifu kuligubika taifa letu,” aliiambia News24.
Alisema Jeshi hilo limefanikiwa kukamata silaha kadhaa ambazo ziliibiwa kwenye vituo vyake na kwamba wanaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine waliokimbia katika mashambulizi yaliyofanyia kanisani hapo.