Chama Cha Demokrasia na Maendeleo kimeeleza kuwa wabunge wake, Halima Mdee (Kawe), Esther Bulaya (Bunda Mjini) na Jesca Kishoa (Viti Maalum) wamelazwa katika hospitali ya Agakhan wakidai kuwa walipigwa na askari polisi walipokuwa nje ya gereza la Segerea wakisubiri kumpokea Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Mkurugenzi wa Itikadi, Uenezi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema amesema kuwa takribani wafuasi 27 wa Chadema walikamatwa jana nje ya gereza hilo.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Zuberi Chembela amesema kuwa jeshi hilo halijawapiga wanachana hao wa Chadema, akieleza kuwa wao wanapaswa kueleza waliowapiga.
“Jukumu la Polisi sio kupiga watu. Hao wanachama wa Chadema hawajapigwa na Polisi labda wawaseme waliowapiga lakini sio polisi,” Kamanda Chembela anakaririwa na Mwananchi.
Mdee na Bulaya waliepuka kifungo cha miezi mitano jela kila mmoja baada ya kulipiwa faini baada ya kukutwa na hatia katika makosa 12 kati ya 13 yaliyokuwa yanawakabili.
Wabunge hao walikuwa miongozi mwa viongozi nane wa chama hicho, ikiwa ni pamoja na Dkt. Vincent Mashinji aliyehamia CCM, waliohukumiwa kwenda jela au kulipa jumla ya Sh. 350 milioni kama faini.