Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amesema kuwa kifo cha Diwani wa Kata ya Namawala tarafa ya Ifakara wilayani Kilombero, Godfrey Joackim (CHADEMA) aliyefariki kwa kukatwakatwa mapanga huenda ni kisasi.

Matei amesema kuwa kiongozi huyo kuna wakati aliwahi kuwaambia wanakijiji ambao walikuwa na ugomvi kati yao na bodi ya sukari, akiwa diwani wa eneo lile alisimamia wananchi kudai lile shamba, ambapo kuna kesi ambayo ipo mahakamani mpaka sasa, lakiniĀ  aliwaambia kuwa kuna mtu anafahamika kwa jina la Kenani Haule ndiye alikuwa anawasaliti hivyo hata kama akiuawa itakuwa sahihi, baada ya muda mtu huyo aliuliwa kwa kukatwakatwa mapanga.

“Mwanzoni mwa mwaka 2016 watu wa Namawala walikuwa na ugomvi kati ya wanakijiji na bodi ya sukari akiwa diwani wa eneo lile alisimamia wananchi wale kudai lile shamba, kwa hiyo diwani Godfrey Joackim aliwaambia kuna mtu anaitwa Kenani Haule ndiye msaliti, hivyo aliwaambia hata kama Kenani akifariki basi wao watakuwa na uwezo wa kupata shamba na kweli muda mfupi Kenani Haule aliuawa kwa kukatwa katwa mapanga tukio ambalo lilitokea kama lilivyotokea kwake,”amesema Matei

Hata hivyo, Kamanda Matei amedai kuwa jeshi la polisi bado linaendelea na uchunguzi na msako mkali unaendelea na kudai hilo ni tukio baya kutokea Morogoro kwa sababu wamempoteza kiongozi wa wananchi wa Namawala na kuwataka wananchi yoyote ambaye anataarifa juu ya mazingira ya mauaji hayo awape taarifa jeshi la polisi ili waweze kuzifanyia kazi zaidi.

 

Video: Wiki ya majonzi, Kigogo Chadema auawa kinyama
Magazeti ya ndani na nje ya Tanzania leo Februari 24, 2018